Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Wanajeshi 32 watiifu kwa serikali ya Libya wameuawa katika makabiliano na kundi la kigaidi la Daesh na katika mashambulizi ya kujitoa mhanga. Hayo yamethibitishwa na jeshi la nchi hiyo ambalo pia limesema watu wengine 50 wamejeruhiwa.
Serikali hiyo ya Libya inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa imesema vikosi vyake vilikuwa vikisonga mbele kuelekea mji wa Sirte, ambao ni ngome kuu ya kundi la kigaidi la Daesh nchini Libya, na kwamba wapiganaji wake waliweza kuikomboa miji mitatu iliyokuwa imetekwa na kundi la kigaidi la Daesh mwanzoni mwa mwezi huu.
Wapiganaji wa kundi hili ndio walikuwa wanatumiwa na Marekani na washirika wake ili kuangusha utawala wa Libya.
Katika mapambano yaliyotokea serikali imewapoteza wapiganaji wake 32, wakiwemo 20 waliouawa katika mripuko wa gari uliosababishwa na mshambuliaji wa kujitoa mhanga kwenye kituo cha ukaguzi wa barabarani cha al-Khamees, kilichoko umbali wa km 50 kutoka mji wa Sirte.
Duru za hospitali ya Misrata, eneo lenye nguvu kubwa kijeshi ambalo linaegemea upande wa serikali ya Umoja wa Kitaifa, zimethibitisha kutokea kwa mashambulizi hayo ya kujitoa mhanga, na idadi ya wanajeshi 20 waliouawa.
Kundi la kigaidi la Daesh yakiri kuhusika
Katika taarifa iliyosambazwa kupitia mitandao ya kijamii, wafuasi wa kundi la kigaidi la Daesh wamedai kuhusika na shambulizi hilo, lakini shirika la habari la DPA halikuweza kuthibitisha madai yao hayo.
Majina ya watu wawili waliotajwa na kundi hilo kufanya mashambulizi ya kujitoa mhanga dhidi ya vikosi vya serikali, yanaashiria kuwa mmoja alikuwa kutoka Sudan, na mwingine kutoka nchi ambayo siyo ya kiislamu.
Miji iliyokombolewa imetajwa kuwa Abugrein, al-Washka na Wadi Zamzam. Shirika la habari la Libya limenukuu vyanzo vya jeshi la serikali, vilivyosema mapigano ya kuikomboa miji hiyo yalijumusha pia wanamgambo wanaoiunga mkono serikali, na operesheni kutoka angani.
Afisa mmoja katika mji wa Abugrein Mohammed al-Jali ameiambia tovuti ya al-Wasat kwamba mashambulizi ya vikosi vitiifu kwa serikali yalikuwa ya kushitukiza, na yaliwalazimisha wapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh kuzikimbia ngome zao, wakiacha nyuma maiti nyingi za wenzao.
Kanali miongoni mwa waliouawa
Ripoti moja imesema katika mapigano ya Jumanne wanajeshi wa serikali wasiopungua sita waliuawa, akiwemo afisa mmoja mwenye cheo cha kanali. Wapiganaji wengine 15 walijeruhiwa katika mapigano hayo, kwa mujibu wa ripoti hiyo.
Libya imetumbukia katika mgogoro wa kivita tangu mwaka 2011, kufuatia vuguvugu la uasi lililomtimua madarakani Muamar Gaddafi, aliyeiongoza kiimla nchi hiyo kwa muda mrefu.
Tangu mwaka 2014, Libya imegawika katika sehemu mbili kuu kiutawala, moja inayotambuliwa kimataifa ikiwa na makao yakew katika mji wa mashariki wa Tobruk, na nyingine yenye mrengo wa kiislamu ikiudhibiti mji mkuu, Tripoli.
Kundi la kigaidi la Daesh ambalo hapo kabla lilikuwa likipewa silaha na Marekani na washirika wake, ili kuangusha utawala wa Gaddafi limenufaika na hali hiyo ya misukosuko, kujiimarisha katika nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa mafuta. Kundi hilo lililochipuka kwa msaada wa Marekani na washirika wake limeweka ngome zake katika mji wa Sirte kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, na zipo taarifa zinazosema limekuwa likiwahamisha maafisa wake na wapiganaji kutoka maeneo yake ndani ya Iraq na Syria , na kuwapeleka Libya baada ya kushindwa vita katika nchi hizo baada ya wataalamu wa vita wa majeshi ya Iran kuingilia kati nakuzisaidia serikali za Syria na Iraq.
Mwisho wa habari/ 291